HUDUMA YA KWANZA KWA MTU ANAYETOKWA DAMU NYINGI.




Habari za leo mpendwa msomaji wa ELIMU YA AFYA!
Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea na majukumu yako ya kulijenga taifa letu, lakini hatuwezi kulijenga taifa vizuri kama tunaona wenzetu wanakufa kwa sababu ya kukosa msaada pale inapotokea ajali aidha ya Baiskeli, Pikipiki, Gari na kadhalika. Ndiyo maana leo nimeamua nikuletee somo hili la namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa mtu aliyepata ajali.

Katika maisha yetu ya kila siku, huwa hatujui ni lini na nani atapata ajali. Ajali hutokea bila kujiandaa na inaweza kumpata mtu yeyote na wakati wowote iwe barabarani, shambani, nyumbani, ofsini na sehemu zingine zoote ambazo sijazitaja. Asilimia kubwa ya watu hawajui kutoa huduma ya kwanza na hivyo kusubiri huduma hiyo itolewe na nesi au daktari. endelea kuwa nami ili upate elimu ya jinsi ya kutoa huduma ya kwanza kwa mgonjwa maana kila mmoja anatakiwa kuwa mstari wa mbele kumsaidia mwingine akipata shida. Kumbuka ukimsaidia mtu yeyote kwa kuokoa maisha yake, MUNGU atakubariki sana.

Leo nitaongelea jinsi ya kumsaidia mtu aliyepata ajali ambayo inasababisha kuvuja kwa damu kidogo au nyingi, aina hii ya ajali mara nyingi sana hutokea kwenye vyombo vya usafiri kama baiskeli, magari, pikipiki, kujikata na kitu chenye ncha kali, kuvamiwa na sababu yeyote nyingine ambayo sijaitaja. Ndiyo maana magari mengi yanakuwa na KISANDUKU CHA HUDUMA YA KWANZA (First Aid Kit).

Huduma ya kwanza ni nini?
Ni matibabu yanayotolewa kwa haraka kwa mtu aliyepata ajali kabla ya kumpeleka hospitali. Lakini pina ni huduma ya dharula ambayo inatakiwa kutolewa na mtu yeyote kama ajali itatokea, Huduma hii inaweza kutolewa lolote.

AJALI INAYOSABABISHA KUVUJA KWA DAMU (HAEMORRHAGE)

Ajali hii inapotokea, mgonjwa anatakiwa kuhudumiwa mapema saana maana akicheleweshewa huduma tu anaweza akafa kama damu itatoka kwa muda mrefu, hii inaweza kusababisha;
  • Mgonjwa kuishiwa nguvu.
  • Mgonjwa kuwa dhaifu (kunyong'onyea)
  • Mgonjwa kupauka (Pallor)
  • Ngozi yake kupata ubaridi.
  • Kupungua kwa msukumo wa damu (Hypotension)
  • Kupumua kwa shida (Shortness of breath)
  • Mgonjwa kupata kizunguzungu.
Naomba nikueleze vitu vya kuwa navyo muda wowote kwenye kisanduku cha huduma ya kwanza ambacho unatakiwa kuwa nacho sehemu yoyote (si kwa wenye magari tu, hata wewe unayetembea kwa mguu maana unaweza kumsaidia mtu yeyote sehemu yoyote). unatakiwa kuwa na vitu vifuatavyo;
  • Mipira ya kuvaa mikononi (Gloves)
  • Bendeji (bandage) 
  • Spirit (70% Alcohol)
  • Pamba (Cotton wool)
  • Gozi (Gauze)
  • Dawa ya kutuliza maumivu
  • mkasi.
 Malengo ya kutoa huduma ya kwanza kwa mgonjwa mwenye tatizo la kutokwa damu ni;
  • Kuzuia damu isiendelee kuisha mwilini.
  • Kuzuia na kupunguza mshtuko wa moyo.
  • Kupunguza maambukizi kwenye kirija ya damu
  • Kumpa msaada mgonjwa kablan na kumpeleka Hospitali mapema kwa ajiri ya matibabu zaidi.
 Jinsi ya kutoa huduma ya kwanza kwa Mtu anayevuja damu kutokana na ajali.
  • Vaa mipira (Gloves) yako mkononi (ili kujikinga namaambukiziya aina yoyote. USIMWAMINI MTU YEYOTE).
  • Kama mgonjwa ana nguo basi zitoe ili kidonda kiwe wazi.
  • Kama kidonda ni kidogo, kioshe kwa maji safi na sabuni halafu tumia vidole vyako kupagandamiza kidogo ukiwa na kipande cha pamba au gozi (gauze) sehemu yenye kidonda ili kupunguza damu kutoka.
  • Kama kidonda ni kikubwa mfano kwenye miguu au kwenye mikono mlaze mgonjwa chini halafu unyanyue juu na uisapoti na kitu chochote sehemu iliyoumia ili kupunguza kasi ya damu kutoka. Weka kipande cha gozi sehemu yenye kidonda na utumie vidole au kiganja cha mkono wako kuzuia damu isiendelee kutoka (hii ifanye kwa muda wa dakika 5 hadi 15 ili damu ya nje igande). Kama mgonjwa anajitambua, mshauri ashike mwenyewe.
  • Funga hiyo sehemu iliyoumia kwa kutumia bandeji baada ya kusafisha na dawa ya kuua wadudu (Antiseptics).
  • Kama damu itaacha kutoka na kama kidonda bado kimechafuka na damu, kioshe kwa maji safi na ukifunge tena kwa bandeji.
  • Kama damu bado inatoka, ongeza kiasi cha gozi na ufunge tena kwa bandeji nyingine juu yake. 
  • ANGALIZO: "Usiifunge sana bandeji kwenye mwili wa mgonjwa maana inaweza kuzuia damu isizunguke maeneo hayo"
  • Wakati unafanya hivi hakikisha sehemu iliyoumia iko juu kidogo zaidi ya kichwa huku mgonjwa akiwa amelala chini au kwenye blanketi (Kama lipo)
  • Usimruhusu mgonjwa kula chochote, kunywa chochote wala kuvuta sigara wakati huu.
  • Baada ya kufanya hivyo, muwahishe mgonjwa hospitali kwa ajiri ya matibabu zaidi.
 MUHIMU;
  • Kama damu inatoka kwa kasi, chunguza vizuri, yawezekana kuna kitu kimebaki mwilini wakati wa ajali kama vile kipande cha chuma, bati au chochote kile,. Jaribu kukitoa lakinik kwa uangalifu sana kisije kikakuchoma na wewe. Kama utashindwa basi mpeleke hospitali kwa madaktari wenye vifaa vya kitaalamu zaidi.
  •  Ikumbukwe kuwa, kama damu itaendelea kutoka kwa muda mrefu, mgonjwa anaweza kupata Shida ya moyo kushindwa kufanya kazi ya kusukuma damu ipasavyo na hata kusababisha kifo.
  
Mpaka hapo nimefikia mwisho wa makala hii. Naamini sasa kila mmoja atanunua vivyaa kwa ajiri ya kutolea huduma ya kwanza na kuviweka nyumbani au kuwa anasafiri navyo popote pale. Tusiwategemee sana madaktari na manesi kwenye huduma hizi maana ni wachache sana na tatizo linaweza kutokea mbali na walipo. Lakini pia tunatakiwa tujue kuwa, wewe ni msaada kwa mtu yeyote yule na pia haujui ni nani atakayekusaidia kama wewe ndiwe utakayepata ajali. kwa hiyo hebu tuishi kwa amani na upendo na jamii tunayokaa nayo na watu tunaosafiri nao.

Kikubwa sana tumtegemee Mungu maana yeye ndiye kila kitu kwetu.

Nakuomba ndugu msomaji uendelee kufuatilia makala zinazofuata hapa www.elimuafya.blogspot.com ili upate elimu mbalimbali za kuhusu afya yako na  ya jamii kwa ujumla.

Jukumu la kutoa huduma ya kwanza ni la kwako wewe na mimi, siyo la manesi na madaktari tu.
  
Emmanuel Shimbala (Lab Tech)

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

VIDONDA VYA TUMBO. (Dalili, Vipimo unavyotakiwa kupima na matibabu yake)

FAHAMU JINSI YA KUTOA HUDUMA YA KWANZA KWA MTU ALIYEZIMIA AU ALIYEPATA MSHTUKO (SHOCK)

FAHAMU MUDA WA KUSUBIRIA MAJIBU YA VIPIMO MBALIMBALI YA MAABARA UKIWA HOSPITALI