VIPIMO UNAVYOTAKIWA KUPIMA KABLA YA KUOA AU KUOLEWA


Habari za leo ndugu msomaji wa makala hii!
Karibu sana kwenye blog hii ya ELIMU YA AFYA ambapo utapata ushauri kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu afya kwa ujumla.

Leo nimeamua kukushirikisha kuhusu vipimo mbalimbali ambavyo unatakiwa kuvipima kabla ya kuingia kwenye mahusiano ya kudumu (uchumba au ndoa), Sasa hivi kuna utaratibu kwenye madhehebu ya dini (karibu yote) ambapo mtu akitaka kuoa au kuolewa ni lazima apimwe afya yake ili kuhakikisha kuwa anayekwenda kuoana naye ana afya nzuri, lakini mara nyingi watu hupima sana sana kipimo kimoja tu ambacho ni HIV Test ambapo kumbe wanasahau kupima vipimo vingine vya muhimu zaidi katika maisha ya ndoa na afya ya watoto kama Mungu atawajaalia.

Vipimo ambavyo kila mmoja anayejiandaa kuingia katika uchumba au ndoa ni vingi sana ambapo nitakueleza baadhi yake. Vipimo vyenyewe ni:
  • Kipimo cha Virusi vya Ukimwi (VVU)
  • Magonjwa ya zinaa.
  • Kipimo cha kuangalia mbegu za mwanaume kama zinaweza kusababisha ujauzito.
  • Ugonjwa wa Sickle cell.
  • Kipimo cha kutambua makundi ya damu.
  • Ultrasound na X-Ray kwa mwanamke. 
Kipimo cha Virusi vya Ukimwi (VVU)

Hiki ni kipimo ambacho asilimia kubwa ya vijana wanapima kabla ya kuingia kwenye uchumba au ndoa. Ni kipimo kinachoweza kutambua uwepo wa virusi vya ukimwi kwenye mzunguko wa damu ya mtu husika.
Hiki kipimo ni muhimu sana kwa wapenzi wanaoingia kwenye hatua nyingine ya uchumba na ndoa.

Faida za hiki kipimo ni
  • Kujua afya zenu.
  • Kuweza kuoa au kuolewa na mtu mwenye afya njema ambaye hana maambukizi ya VVU.
  • Kutengeneza familia yenye afya njema kwa kuwa na watoto wenye afya njema.
  • Kupanga malengo ya muda mrefu katika familia mtakayoianzisha.
  • Kama mtu mmoja au wote mmeathirika, mtaanza matibabu mapema na kupata ushauri wa namna ya kuishi ukiwa na Virusi vya ukimwi.
Hasara za kupima kipimo hiki.

Kama utagundulika na VVU baada ya kupima;
  • Unaweza kuachana na mchumba wako ambaye ulipanga kuishi naye.
  • Unaweza kuishi kwa kujinyanyapaa au kukosa ushirikiano kwa ndugu unaoishi nao.
  • Utaishi kwa kutegea dawa kila siku.
  • Kuhudhulia Hospitali au kituo cha afya mara kwa mara ili kuendelea kupata ushauri kwa Afya yako.

Magonjwa ya zinaa.

Kipimo hiki husahaulika sana kwa wachumba lakini ni cha muhimu sana wakati wa kujiandaa kuingia katika uchumba au ndoa. Tunapima hiki kipimo wakati huu ili kujua kama mmeathirika na magonjwa ya zinaa kwa maana kuna baadhi ya magonjwa haya huharibu mfumo wa uzazi kwa mwanamke na mwanamme na hivyo kupelekea kutokupata watoto.

Faida za hiki kipimo ni:
  • Kujitambua mapema kama una maambukizi ya magonjwa ya zinaa na kutibiwa mapema.
  • Kupata ushauri na njia sahihi za kujikinga na maambukizi ya magonjwa ya zinaa.


Kipimo cha kuangalia mbegu za mwanaume kama zinaweza kusababisha ujauzito. (SEMINALYSIS)

Hiki ni kipimo ambacho mbegu (shahawa) za mwanaume hupimwa maabara kama zina uwezo wa kusababisha ujauzito kwa mwanamke. Kipimo hiki ni muhimu sana maana ndoa nyingi sana huvunjika kwa kukosa watoto ambapo tatizo linaweza kuwa kwa mwanamme ambaye mbegu zake hazina uwezo wa kusababisha ujauzito. Hili ni tatizo kubwa sana kwenye jamii zetu za kiafrika ambapo kama tatizo hili litatokea, mara nyingi lawama zinakwenda kwa mwanamke na mwisho wake ni ndoa kuvunjika.

Tatizo hili linaweza kuwa ni la kuzaliwa nalo au limesababishwa na magonjwa ambayo yanaweza kutibika. Kama tatizo ni la kuzaliwa nalo, hakuna njia ya kulitibu lakini kama tatizo ni la kusababishwa na magonjwa basi linaweza kutibika na mwanaume akaendelea kuzalisha mbegu zenye uwezo mzuri wa kuzalisha.

Katika kipimo hiki, mwanaume anatakiwa asifanye tendo la ndoa kwa muda wa siku tatu hadi tano ili kuruhusu utengenezwaji wa manii nyingi.

Faida za hiki kipimo ni:
  • Mwanamme atakuwa na uhakika wa kutoa mbegu zenye ubora na zenye uwezo wa kutungisha mimba.
  • Kuwa na uhakika wa kupata watoto.

Ugonjwa wa Sickle cell.

Hiki kipimo pia huwa kinasahaulika sana wakati wa maandalizi ya kufunga ndoa
Kipimo hiki hupimwa maabara ili kutambua uwepo wa ugonjwa wa Sickle Cell. Ugonjwa wa Sickle Cell ni ugonjwa wa kurithi, aidha kutoka kwa wazazi wote (Sickle cell anaemia) au kutoka kwa mzazi mmoja (Sickle Cell Trait). 

Kwenye mwili wa binadamu kuna chembe nyekundu za damu (RBCs) ambazo huwa zinazunguka mwilini mwote kwa muda wa siku 110-120 na baada ya muda huo hizo chembe nyekundu hufa, hii inakuwa tofauti sana kwa mtu mwenye ugonjwa wa Sickle Cell ambapo chembe nyekundu za damu hufa kabla ya muda wake na mwisho husababisha upungufu wa damu.

Ni muhimu sana kupima ugonjwa huu kabla ya kuoa au kuolewa ili kuzuia tatizo la baadae kupata mtoto mwenye ugonjwa wa sickle Cell ambapo itakuja kuwagharimu saana katika kumuongezea damu mara kwa mara. Kutokuzingatia hili kwaweza kusababisha poromoko la uchumi katika familia yako baadae na pia kusababisha kifo/vifo kwa sababu ya kuishiwa na damu mara kwa mara.


 Kipimo cha kutambua makundi ya damu.

 Mwili wa binadamu umeundwa kwa chembechembe za damu. Kila mwanadamu ana kundi lake la damu ambapo kuna makundi makuu manne ya damu Duniani ambapo kila mmoja wetu ana kundi mojawapo katika haya manne. Makundi haya ya damu ni;
  • kundi A,
  • kundi B,
  • Kundi AB na
  • kundi O
 Kila kundi la damu hapo juu lina Rhesus factor abayo inaweza kuwa Chanya(+) au hasi (-). Kila mtu anarithi kutoka kwa wazazi wake kundi la damu na Rhesus Factor.

Kama mwanamke mwenye Rhesus Factor hasi(Negative)ataoana na mwanamme mwenye Rhesus Factor Chanya (positive), na kama atapata mimba na mtoto wa tumboni akarithi Rhesus Factor kutoka kwa baba ambayo ni positive, kuna uwezekano wa mama kukomea kuzaa mtoto mmoja tu maisha yake yote au hata huyo mmoja akampoteza wakati wa kujifungua kwa sababu hasi na chanya hukutana na kwenye damu hasi na chanya zikikutana huleta madhara makubwa kwa hiyo hili tatizo linatakiwa kutatuliwa kabla ya kuingia katika mahusiano.



 Ultrasound na X-Ray kwa mwanamke. 

Hapo juu nimeelezea kuhusu kipimo kwa mwanaume cha kuangalia kama ana uwezo wa kusababisha ujauzito (mimba), sasa nahamia kwa mwanamke, Mara nyingi sana tunajisahau kupima vipimo vya kututambulisha kama huyu mwanamke ana uwezo wa kubeba mimba.

Matatizo mengi ya kutokubeba ujauzito kwa wanawake husababishwa na mirija ya uzazi kuziba (Fallopian tubes) na uvimbe kwenye  mfuko wa uzazi (Placenta). ili kujua kama kuna matatizo hayo, ni lazima mwanamke anayetaka kufunga ndoa apimwe ULTRASOUND na X-Ray.

Hapa ndiyo mwisho wa  somo langu la leo ambalo limejikita kwa vijana wanaotaka kuingia kwenye mahusiano ya mume na mke. Ewe mzazi, mlezi kiongozi wa dini au wa serikari, naomba tushirikiane kutoa elimu hii kwa vijana wetu ili baadaye tuweze kupata taifa lenye watu walio na afya njema kutokana na kupata mke/mme mwenye afya bora.

Kumbuka kuwa  Ndoa yenye afya bora huzaa watoto wenye afya bora ambao watakuwa viongozi bora kwenye kanisa na jamii kwa ujumla.



Nakuomba usisahau kufuatilia mafundisho yangu mbalimbali yatakayokujia mara kwa mara kupitia blog hii ya ELIMU YA AFYA.


Na Emmanuel Shimbala. 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

VIDONDA VYA TUMBO. (Dalili, Vipimo unavyotakiwa kupima na matibabu yake)

FAHAMU JINSI YA KUTOA HUDUMA YA KWANZA KWA MTU ALIYEZIMIA AU ALIYEPATA MSHTUKO (SHOCK)

FAHAMU MUDA WA KUSUBIRIA MAJIBU YA VIPIMO MBALIMBALI YA MAABARA UKIWA HOSPITALI