Sehemu ya kwanza: MAMBO YA KUZINGATIA WAKATI WA KUANDAA SAMPULI KWA AJIRI YA UCHUNGUZI ZAIDI MAABARA

Ni matumaini yangu kuwa hujambo mpedwa msomaji wa makala hii.

Karibu sana tena kwenye maada ya leo ambapo nitakueleza mambo ya kuzingatia wakati wa kuandaa sampuli utakachokipeleka maabara kwa ajiri ya uchunguzi zaidi. Vipimo vya maabara vinachangia sehemu kubwa sana katika matibabu ya mgonjwa yeyote, kwa hiyo ni vyema sana kila mgonjwa akapata vipimo sahihi kutokana na jinsi anavyojisikia,

kwanza kabisa naomba tukumbushane kuwa, mgonjwa anapokwenda Hospitali kutibiwa, ana haki ya kupata vipimo kutokana na dalili zake (Hapa mgonjwa anatakiwa kumweleza daktari bila kuficha tatizo lake linalomsumbua ili daktari aweze kumtibu vyema). Kwa kufanya hivyo Mgonjwa atapata matibabu sahihi.

Pia, Mgonjwa anatakiwa kufuata masharti atakayopewa na daktari kuhusu vipimo alivyoandikiwa kupima.

SAMPULI ni sehemu ndogo ya majimaji ya mwilini, haja kubwa, mkojo, makohozi, na vingine kutoka kwa mtu/mgonjwa ambavyo vinastahili kufanyiwa uchunguzi na mtaalamu wa maabara ili kuweza kubaini au kugundua tatizo la mtu/mgonjwa husika.

Kuna njia mbili za ukusanyaji wa sampuli katika Maabara kwa ajiri ya kufanyia uchunguzi ambazo ni;
  • Kukusanya kupitia mtaalamu wa afya mwenye utaalamu. Ukusanyaji huu hufanywa na mtaalamu wa maabara, nesi au daktari kwa vipimo vya Damu, Majimaji ya kwenye uti wa mgongo (ili kuangalia maambukizi katika uti wa mgongo), Usaha kwesye sehemu yoyote mwilini, kipande au vipande vya ngozi ama sehemu yoyote ya mwili na kipimo chochote kinachohusu majimaji ya binadamu.
  • Mgonjwa mwenyewe. Kuna vipimo ambavyo mgonjwa mwenyewe ni lazima avikusanye na kuvipeleka maabara. Vipimo hivyo ni; Makohozi, Haja kubwa (kinyesi), Mkojo, Shahawa.
Leo sitaongelea kuhusu sampuli vinavyokusanywa na mtaalamu wa afya bali nitasema kuhusu sampuli vinavyokusanywa na mgonjwa mwenyewe.

Mambo ya kuzingatia wakati wa kuandaa sampuli (zinazoandaliwa na mgonjwa mwenyewe) kwa ajiri ya uchunguzi wa kitaalamu ni kama ifuatavyo;

Mkojo.

Ni kipimo kinachopimwa Maabara ili kutambua wadudu au bakteria wanaosababisha kuathirika kwa njia ya mkojo na figo, lakini pia kutambua kama mgonjwa ameathirika na wadudu wanaosababisha kichocho.
Kipimo hiki kinachukuliwa na mgonjwa mwenyewe baada ya kupewa na mtaalamu wa Maabara,Nesi au Daktari kifaa cha kuchukulia. Ili kuchukua hiki kipimo:
  • Tumia chupa au kifaa utakachopewa Hospitali kuchukua sampuli ya mkojo kwa ajiri ya kufanyiwa uchunguzi.
  • Kojoa ndani ya chupa, jitahidi ili mkojo usisambae nje ya chupa. Hii ni kwa sababu ya kumkinga atakayekupokea kuupeleka Maabara (kama siyo wewe utakayepeleka) na mpimaji na maambukizi yanayotokana na bakteria au wadudu wanaoweza kupatikana kwenye mkojo. wadudu hao wanaweza kusababisha kichocho ama matatizo kwenye njia ya mkojo.
  • Peleka sampuli ya mkojo mara moja  Maabara baada tu ya kuweka kwenye kifaa husika na kuifunika vizuri. Hii sampuli inatakiwa kupelekwa Maabara ndani ya masaa mawili baada ya kuukusanya ili kama kuna mayai ya kichocho ndani yake yaweze kuonekana. Ukichelewesha unaweza kusababisha Mtaalamu wa maabara kushindwa kuonna haya mayai kwa sababu yanaweza kufa na kutoonekana kabisa.
  • Baada ya kupeleka sampuli yako maabara, mtaalamu wa Maabara atakuambia kuhusu muda wa kusubiria majibu najinsi ya kuyapata majibu yako.
Makohozi.

Ni kipimo kinachopimwa Maabara ili kutambua uwepo wa vimelea vya wadudu wanaosababisha Kifua Kikuu.
Kipimo hiki kinachukuliwa na mgonjwa mwenyewe baada ya kupewa na mtaalamu wa Maabara,Nesi au Daktari kifaa cha kuchukulia. Ili kuchukua hiki kipimo:
  • Tumia chupa au kifaa utakachopewa Hospitali kuchukua sampuli ya makohozi kwa ajiri ya kufanyiwa uchunguzi. 
  • Achama kidogo ukiwa umetazama juu kidogo halafu uvute pumzi kwa nguvu, Kohoa kwa nguvu halafu makohozi uliyyokohoa uyaweke kwenye chupa au kifaa ulichopewa na mtaalamu wa Maabara.
  • Tema makohozi ndani ya chupa au kifaa ulichopewa na mtaalamu na usiteme nje ya chupa ili kupunguza maambukizi ya Kifua kikuu kwuenea kwa wengine.
  • Funika vizuri hiyo sampuli na uipeleke moja kwa moja maabara.
  • Utaratibu wa kuchukua sampuli hii ni kurudia mara mbili yaani Ukifika Hospitali utapewa kopo ukalete sampuli na baada ya kuleta sampuli ya kwanza utapewa kopo jingine kwa ajiri ya kukusanya tena sampuli nyingine asubuhi. Hii ni kwa sehemu ambazo wanapima kwa kutumia darubini, lakini utaambiwa kuleta makohozi mara moja tu  kama kipimo hiki kitapimwa kwa kutumia mashine za kisasa zaidi (Gene X-Part) 
  • Baada ya kupeleka sampuli yako maabara, mtaalamu wa Maabara atakuambia kuhusu muda wa kusubiria majibu na jinsi ya kuyapata majibu yako. 
Kinyesi (Haja kubwa)

Ni kipimo kinachopimwa Maabara ili kutambua uwepo wa minyoo na wadudu wanaosababisha homa ya matumbo (Typhoid fever)
Kipimo hiki kinachukuliwa na mgonjwa mwenyewe baada ya kupewa na mtaalamu wa Maabara,Nesi au Daktari kifaa cha kuchukulia. Ili kuchukua hiki kipimo:
  • Tumia chupa au kifaa utakachopewa Hospitali kuchukua sampuli ya kinyesi kwa ajiri ya kufanyiwa uchunguzi.
  • Weka ndani ya chupa sehemu kidogo ya kinyesi (kama gramu moja hivi).
  • Peleka sampuli uliyokusanya mara moja  Maabara baada tu ya kuweka kwenye kifaa husika na kuifunika vizuri. Hii sampuli inatakiwa kupelekwa Maabara ndani ya masaa mawili baada ya kuukusanya ili kama kuna mayai au minyoo ndani yake viweze kuonekana. Ukichelewesha unaweza kusababisha Mtaalamu wa maabara kushindwa kuona mayai  au minyoo kwa sababu vinaweza kufa na kutoonekana kabisa.
  • Baada ya kupeleka sampuli yako maabara, mtaalamu wa Maabara atakuambia kuhusu muda wa kusubiria majibu na jinsi ya kuyapata majibu yako. 
Shahawa. 

Hiki nii kipimo kinachopimwa Maabara (kwa mwanaume) ili kutambua kama ana uwezo wa kuzalisha (Fertility)
Kipimo hiki kinachukuliwa na mgonjwa mwenyewe baada ya kupewa na mtaalamu wa Maabara,Nesi au Daktari kifaa cha kuchukulia. Ili kuchukua hiki kipimo:
  • Mwanaume anatakiwa kukaa siku  tatu hadi tano bila kufanya tendo la ndoa ili aweze kupata majibu mazuri zaidi ya kipimo hiki.
  • Tumia chupa au kifaa utakachopewa Hospitali kuchukua sampuli ya shahawa kwa ajiri ya kufanyiwa uchunguzi. 
  • Kuna njia mbili za kukusanya sampuli hii ambazo ni kwa njia ya kujichua na njia nyingine ni kwenda na mwenzi wako wa ndoa, mfanye tendo la ndoa na baadaye unamwaga mbegu zako kwenye kichupa au kifaa ulichopewa na mtaalamu wa Maabara. Njia zote hizi zinatoa majibu mazuri sana.
  • Funika sampuli yako na uipeleke mara moja maabara ndani ya saa moja baada ya kukusanya maana mbegu za kiume zinaweza kufa kama zitakaa nje ya joto la mwili kwa muda mrefu.
  • Baada ya kupeleka sampuli yako maabara, mtaalamu wa Maabara atakuambia kuhusu muda wa kusubiria majibu na jinsi ya kuyapata majibu yako. 
Baada ya kupeleka sampuli yako maabara, una haki ya kumuuliza mtaalamu wako wa maabara kuhusu muda wa kuchukua majibu.

Baada ya kukujuza hayo, nakuomba uendelee kufuatilia machapisho yanayokuja kupitia www.elimuafya.blogs.com ili ufahamu zaidi kuhusu afya yako. Lakini pia unaweza kujisajiri kwa kutumia email address yako ili uweze kupata moja kwa moja kila kinachokuja kipya.

Asante sana

Mimi Emmanuel Shimbala (Lab Tech)

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

VIDONDA VYA TUMBO. (Dalili, Vipimo unavyotakiwa kupima na matibabu yake)

FAHAMU JINSI YA KUTOA HUDUMA YA KWANZA KWA MTU ALIYEZIMIA AU ALIYEPATA MSHTUKO (SHOCK)

FAHAMU MUDA WA KUSUBIRIA MAJIBU YA VIPIMO MBALIMBALI YA MAABARA UKIWA HOSPITALI